Social Icons

Wednesday 8 July 2015

Sterling Agomea Ziara Ya Liverpool Ya Mashariki Ya Mbali


Sasa Raheem Sterling amemwonyesha Brendan Rodgers wazi wazi nia yake ni kulazimisha Uhamisho kwenda Manchester City baada kumtaka Meneja huyo kumwacha kwenye Ziara ya Liverpool ya huko Mashariki ya Mbali na Australia.

 Tangu arejee toka Vakesheni na kuanza Mazoezi Juzi Jumatatu, Sterling amefanya mazungumzo na Brendan Rodgers na kusisitiza msimamo wake wa kuihama Liverpool hivi sasa na pia kutaka asiwemo kwenye Ziara ya Wiki mbili ya Liverpool ya huko Thailand, Australia na Malaysia ambayo wanatarajiwa kurejea Julai 25.
 
Msimamo huu mkali ni mwendelezo wa mvutano wa Mchezaji huyo na Liverpool ulioanza Msimu uliopita baada ya kugomea Mkataba mpya wa nyongeza ambao ungempa Mshahara wa Pauni 100,000 kwa Wiki badala ya Mkataba wa sasa, unaompa 35,000 kwa Wiki, ambao unakwisha Miaka Miwili ijayo.
Inaaminika Sterling anataka kuhamia Man City ambao tayari wameshatoa Ofa mbili kwa Liverpool za kumnunua na zote kukataliwa.
 
Ofa hizo za City ni zile za Pauni Milioni 25, inayopanda hadi Milioni 30, na ya pili ni Pauni Milioni 35 inayopanda hadi Milioni 40 kufuatana na mafanikio ya Mchezaji huyo.
 
Habari toka ndani ya Liverpool zinadai Klabu hiyo inamthamini Sterling kuwa na thamani ya Uhamisho ya Pauni Milioni 50 na pia ikijua kuwa Dau lolote la kumuuza lazima Klabu ya Sterling ya zamani, Queens Park Rangers, inapaswa kulipwa Asilimia 20 ya kitita hicho.
 
Hata hivyo, Brendan Rodgers anatarajia kusafiri na Raheem Sterling na Mchezaji huyo kucheza Mechi yao ya kwanza huko Bangkok Jumanne ijayo endapo atamchagua.
 
Rodgers ana uzoefu wa hali kama hii kwani Mwaka 2013 walisafiri na Luis Suarez kwenda huko Australia kabla Msimu kuanza licha ya Mchezaji huyo kung'ang'ani kuhama.

No comments:

Post a Comment