Social Icons

Friday, 18 October 2013

Misri yaafiki Ethiopia kujenga bwawa Mto Nile


Afisa mmoja wa Misri amesema kuwa serikali ya mpito ya nchi hiyo imeafiki uamuzi wa Ethiopia kujenga bwawa katika Mto Nile. Gazeti la al Sha'ab al Jadid huku likimnukuu afisa huyo limeandika kuwa, baada ya kukubali mabadiliko yaliyofanywa na Ethiopia kuhusu ujenzi wa bwawa la an Nahdha katika Mto Nile, serikali ya mpito ya Misri imeafiki ujenzi huo. Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesisitiza kuwa, hata hivyo bado haijajulikana muda wa kufanyika kikao cha Mawaziri wa Maji wa Misri, Sudan na Ethiopia kwa ajili ya kujadili ripoti ya mwisho ya kamati ya kimataifa kuhusu matokeo na athari za kujengwa bwawa hilo kwa usalama wa maji ya Misri na Sudan.
Itakumbukwa kuwa, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, baada ya kuonana na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Sudan pambizoni mwa mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York alipendekeza kushiriki Misri katika ujenzi wa bwawa hilo, na serikali ya Cairo ilikubali pendekezo hilo.

No comments:

Post a Comment