Sunday 11 May 2014
Ngorongoro Heroes Yachapwa 2-0 Kavu dhidi ya Nigeria
Timu ya soka ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo imejiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika mwakani nchini Senegal, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Nigeria Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipa namba moja na Nahodha, Aishi Salum Manula alidaka kwa dakika 45 bila kufungwa, lakini alishindwa kurejea kumalizia mchezo baada ya kuumia dakika za mwisho za kipindi cha kwanza.
Kipa wa pili, Peter Manyika Peter alifungwa bao la kwanza dakika ya tano tu tangu aingie na Yahya Musa, aliyemalizia krosi ya chinichini ya Muhamed Musa dakika ya 50.Ngorongoro ikacharuka baada ya bao hilo na kuanza kushambulia mfululizo langoni mwa Flying Eagles, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi kadhaa.Mshambuliaji Juma Luizio aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Gadiel Michael alishindwa kuiongezea uhai timu kama ilivyotarajiwa na badala yake, Saad Kipanga aliendelea kuhangaika mwenyewe.Wakati Ngorongoro ikiwa katika harakati za kusaka bao la kusawazisha, Nigeria walifanya shambulizi la kushitukiza na kufanikiwa kupata bao la pili, lililoinyong’onyesha kabisa Tanzania.
Bao hilo lilifungwa na Awoinyi Taiwo baada ya kutumia vizuri makosa ya beki Pato Ngonyani aliyechelewa kuondosha mpira kwenye eneo la hatari.Kwa matokeo hayo, Ngorongoro itatakiwa kushinda mabao 3-0 ugenini Mei 23 ili kusonga mbele, au ishinde 2-0 na mshindi wa jumla aamuliwe kwa mikwaju ya penalti.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula/Peter Manyika dk46, Swaleh Mohamed/Mohamed Ibrahim dk63, Mohammed Hussein, Pato Ngonyani, Abdallah Kheri, Abdi Banda, Ally Nassor, Kevin Friday, Saad Kipanga, Idd Suleiman na Gadiel Michael/Juma Luizio dk46.
Nigeria; Enahold Joshua, Muhamed Musa, Mustapha Abdullahi, Idowu Akinjide, Ndidi Onyinye Wilfred, Omego Prince Izuchukwu, Alfa Abdullah, Abdullah Alhassan/Iheanacho Promise dk46, Awonyi Taiwo, Mathew Ifeanyi na Yahya Mussa/Nwakali Chidiebere dk74.
Labels:
AddyTz
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment